Monday, 1 December 2008

SHEIN AASA WASIO NA UKIMWI WASIAMBUKIZWE

Na Mwandishi Maalumu, Kigoma
MAKAMU wa Rais, Dkt. Ali Mohammed Shein, amesema moja ya changamoto kubwa zinazowakabili Watanzania katika vita dhidi ya UKIMWI, ni kuhakikisha asilimia 94.2 ya waliokuwa hawajaambukizwa virusi wanabaki salama. Ameongeza kuwa hilo linaweza kufanikiwa endapo tu Watanzania ambao kwa mujibu wa utafiti mbalimbali asilimia 98 kati yao wanaoufahamu ugonjwa huo, watabadili tabia na kuepuka vitendo vinavyosababisha maambukizi mapya. Akizungumza jana kwenye maadhimisho ya Siku ya UKIMWI duniani, yaliyofanyika kwenye uwanja wa Lake Tanganyika mjini hapa, Dkt. Shein alisisitiza kuwa
hakuna njia nyingine ya kuliweka Taifa salama dhidi ya ugonjwa huo, bila jamii kubadili tabia. Alishauri jitihada za kupambana na ugonjwa huo ziende sambamba na kutilia mkazo suala la kuondoa tofauti katika jamii na utendaji haki ili kuepusha maambukizi mapya. Dkt. Shein alinukuu utafiti uliofanywa mwaka 2007/8 kuwa kiwango cha maambukizi kitaifa kimeshuka hadi asilimia 5.8 kutoka asilimia 7 mwaka 2003/4. Hata hivyo, alionya kuwa kiwango hicho bado ni kikubwa hivyo Watanzania hawana budi kulenga kukipunguza zaidi. Akizungumzia kaulimbiu ya mwaka huu ya “ZUIA UKIMWI TIMIZA AHADI: ONGOZA, WEZESHA NA TIMIZA,” Dkt. Shein alisema kauli hiyo inampa changamoto kila kiongozi wa Serikali, idara na taasisi zake, kuhakikisha kuwa anapanga na kutekeleza mipango ya kupambana na ugonjwa huo katika sehemu anayoongoza. Alitahadharisha matumizi mabaya ya fedha zinazotolewa kwa ajili ya shughuli za mapambano dhidi ya ugonjwa huo na kueleza kuwa Serikali haitawafumbia macho watakaohusika na matumizi hayo.

No comments: